Skip to content

Yesu Anaomba Atukuzwe

17 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, alitazama mbinguni akasema,

“Baba, wakati umefika. Dhihirisha utukufu wangu ili nami nikutukuze wewe, kwa kuwa umenipa mamlaka juu ya watu wote, niwape uzima wa milele wale ambao umewakabidhi kwangu. Na huu ndio uzima wa milele: wakufahamu wewe ambaye pekee ni Mungu wa kweli, nakumfah amu Yesu Kristo ambaye umemtuma. Baba nime kutukuza hapa duniani kwa kutimiza kazi uliyonipa niifanye. Na sasa Baba nipe mbele yako ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe hata kabla dunia haijaumbwa.

Yesu Anawaombea Wanafunzi Wake

Nimewafahamisha jina lako wale ambao umenipa kutoka katika ulimwengu. Wao wametii neno lako. Sasa wamefahamu ya kuwa vyote ulivyonipa vinatoka kwako ; kwa kuwa nimewapa ujumbe ulionipa, nao wameupokea. Wamefahamu hakika ya kuwa nimetoka kwako na wameamini kwamba ulinituma. Siwaombei watu wote wa ulimwengu bali nawaombea hawa ulionipa kwa sababu wao ni wako. 10 Wote ulionipa ni wako, na walio wako ni wangu; nao wanadhihirisha utukufu wangu. 11 Mimi naondoka ulimwenguni ninakuja kwako. Lakini wao wako ulimwenguni. Baba Mtakatifu, walinde kwa jina lako ambalo umenipa ili wawe na umoja kama sisi tulivyo mmoja. 12 Nilipokuwa pamoja nao niliwalinda wakawa salama kwa uwezo wa jina ulilonipa. Nimewalinda na hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyeamua kupotea, ili Maandiko yapate kutimia.

13 Lakini sasa nakuja kwako na ninasema haya wakati nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kikamil ifu. 14 Nimewapa neno lako na ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao, kama mimi, si wa ulimwengu huu. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde na yule mwovu shetani. 16 Kama mimi nisivyo mwenyeji wa ulimwengu huu, wao pia sio wa ulimwengu. 17 Watakase kwa neno lako; kwa maana neno lako ndilo kweli. 18 Kama ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma wao ulim wenguni. 19 Kwa ajili yao nimejitoa wakfu kwako ili na wao wapate kuwa watakatifu kwa kufahamu kweli yako.

Yesu Anawaombea Waamini Wote

20 “Siwaombei hawa peke yao; bali nawaombea pia wale wote watakaoniamini kwa sababu ya ushuhuda wa hawa. 21 Ninawaombea wote wawe kitu kimoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi ni ndani yako; ili na wao wawe ndani yetu na ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ulinituma. 22 Nimewapa utukufu ule ule ulionipa ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo – 23 mimi nikiwa ndani yao na wewe ndani yangu; ili wakamilike katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma na kwamba unawapenda kama unavyonipenda mimi.

24 Baba, shauku yangu ni kwamba, hawa watu ulionipa wawepo mahali nilipo ili waweze kuona utukufu wangu; utukufu ambao umenipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ulimwengu haujaumbwa.

25 Baba Mtakatifu, ijapokuwa ulimwengu haukufahamu wewe, mimi ninakufahamu, na hawa wanajua ya kuwa umenituma. 26 Nimekutambulisha wewe kwao, na nitaendelea kulitambulisha jina lako kwao ili upendo ulio nao kwangu uwe upendo wao pia; nami niwe ndani yao.”