Skip to content

41 Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.

42 Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akapeleka mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zako Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua. 43 Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani; 44 ukae kwake siku chache, hata ghadhabu ya ndugu yako igeuke; 45 hata ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapopeleka watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja?

46 Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yatanifaidia nini?

28 Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako. Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila. Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Ibrahimu. Basi Isaka akampeleka Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.