28 Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; 2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.
3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.
6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo.
7 Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
8 Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.
9 Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya Bwana, Mungu wako, na kutembea katika njia zake. 10 Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la Bwana, nao watakuwa na hofu kwako. 11 Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.
12 Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe. 13 Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya; 14 msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lo lote, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.
Laana kwa Kutokutii
15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.
16 Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.
17 Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.
18 Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
19 Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,
20 Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo. 21 Bwana atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki. 22 Bwana atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie. 23 Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma. 24 Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.
25 Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani. 26 Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza. 27 Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa. 28 Bwana atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni; 29 utakwenda kwa kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.
30 Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake. 31 Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang’anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa. 32 Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako. 33 Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima; 34 hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona. 35 Bwana atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.
36 Bwana atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe. 37 Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza Bwana.
38 Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila. 39 Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu. 40 Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika. 41 Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani. 42 Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.
43 Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini. 44 Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.
45 Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza; 46 nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele; 47 kwa kuwa hukumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote; 48 kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
49 Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake; 50 taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana; 51 naye atakula uzao wa ng’ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng’ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza. 52 Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa Bwana, Mungu wako.
53 Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa Bwana, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako. 54 Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye; 55 hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote. 56 Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatirisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake, 57 na juu ya mchanga wake atokaye katikati ya miguu yake, na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako.
58 Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, Bwana, MUNGU WAKO; 59 ndipo atakapofanya Bwana mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana. 60 Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe. 61 Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha torati hii, atakutia nayo Bwana juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa. 62 Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako. 63 Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi Bwana juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi Bwana juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki.
64 Bwana atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe. 65 Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini Bwana atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika; 66 na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako; 67 asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona. 68 Bwana atakurudisha tena Misri kwa merikebu, kwa njia ambayo nilikuambia, Hutaiona tena po pote; nanyi huko mtajiuza nafsi zenu kwa adui zenu kuwa watumwa na wajakazi, wala hapana atakayewanunua.
Kufanywa upya kwa Agano
29 Haya ndiyo maneno ya agano Bwana alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu.
2 Musa akawaita Israeli wote akawaambia,
Mmeyaona yote Bwana aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote; 3 yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu; 4 lakini Bwana hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi. 5 Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako. 6 Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
7 Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga; 8 tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase, iwe urithi.
9 Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo. 10 Leo mmesimama nyote mbele za Bwana, Mungu wenu; wakuu wenu, na kabila zenu, na wazee wenu, na maakida wenu, waume wote wa Israeli, 11 vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako; 12 ili uingie katika agano la Bwana, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe Bwana, Mungu wako, hivi leo; 13 apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. 14 Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki; 15 ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya Bwana, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo;
16 (kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao; 17 nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;) 18 asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache Bwana, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga;
19 ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu kwa kuangamiza mbichi na kavu; 20 Bwana hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya Bwana na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na Bwana atalifuta jina lake chini ya mbingu. 21 Bwana atamtenga kwa uovu, kutoka kabila zote za Israeli, kwa laana zote za agano lililoandikwa katika chuo hiki cha torati.
22 Na kizazi cha baadaye, wanenu watakaoinuka baada yenu, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watasema, watakapoyaona mapigo ya nchi ile, na magonjwa aliyoitia Bwana; 23 ya kuwa nchi yake nzima ni kibiriti, na chumvi, na kuteketea, haipandwi, wala haizai, wala nyasi hazimei humo, kama mapinduko ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, aliyoipindua Bwana kwa ghadhabu yake na hasira zake; 24 mataifa yote watasema, Mbona Bwana ameifanyia hivi nchi hii? Ni nini maana yake hari ya hasira hizi kubwa?
25 Ndipo watakaposema watu, Ni kwa kuwa waliacha agano la Bwana, Mungu wa baba zao, alilofanya nao hapo alipowatoa katika nchi ya Misri; 26 wakaenda wakatumikia miungu mingine, wakaiabudu miungu wasiyoijua, asiyowapa yeye; 27 ndipo ikawashwa hasira ya Bwana juu ya nchi hii, kwa kuleta juu yake laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki; 28 Bwana akawang’oa katika nchi yao kwa hasira, na ghadhabu, na makamio makuu, akawatupa waende nchi nyingine, kama hivi leo.
29 Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.
Mafanikio Baada ya Kumgeukia Bwana
30 Tena itakuwa, mambo haya yote yatakapokujilia, baraka na laana nilizoweka mbele yako, nawe utakapozikumbuka kati ya mataifa yote, huko atakakokupeleka Bwana, Mungu wako, 2 nawe utakapomrudia Bwana, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; 3 ndipo Bwana, Mungu wako, atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia, tena atarejea na kukukusanya kutoka mataifa yote, huko alikokutawanyia Bwana, Mungu wako. 4 Watu wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko atakukusanya Bwana, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa; 5 atakuleta Bwana, Mungu wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako. 6 Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai. 7 Na laana hizi zote Bwana, Mungu wako, atawatia adui zako na hao wakuchukiao, waliokuwa wakikutesa. 8 Nawe utarudi, uitii sauti ya Bwana, na kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo. 9 Na Bwana, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng’ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa Bwana atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako; 10 ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.
Sadaka ya Uhai au Kifo
11 Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali. 12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya? 13 Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya? 14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
15 Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; 16 kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki.
17 Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; 18 nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki.
19 Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; 20 kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.