Maji Kutoka Mwambani
17 Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama Bwana alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe. 2 Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe.
Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu Bwana?
3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?
4 Musa akamlilia Bwana, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe.
5 Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. 6 Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. 7 Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?